Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Mapinduzi makubwa katika sekta ya Miundombinu ya Bandari yanalenga kuifanya Zanzibar kuwa kituo muhimu cha Usafirishaji na kupokea Meli kubwa zinazoleta bidhaa nchini.
Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 18 Oktoba 2024 alipoifungua Bandari kavu ya Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amefahamisha kuwa ufunguzi wa Bandari kavu ni hatua muhimu ya kuimarisha utendaji wa bandari kwani itapunguza msongamano wa makontena katika Bandari ya Malindi.
Rais Dk. Mwinyi ameeleza, mabadiliko hayo ya Miundombinu ya Bandari yataleta msukumo mkubwa wa ukuaji wa Uchumi wa Zanzibar na kuwasisitiza wadau kuunga mkono juhudi hizo.
Halikadhalika Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa kampuni ya Africa Global Logistic inayoendesha bandari ya Malindi hivi sasa inaendelea kuleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji yanayoongeza Ufanisi na kuwapa urahisi Wafanyabiashara kutekeleza wajibu wao bila usumbufu pamoja na kuokoa muda.
Kwa upande mwingine, Rais Dk. Mwinyi amewahakikishia wadau kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kufanya kazi zaidi na sekta binafsi kwani mbali ya kuja na mitaji, pia wanakuja na utaalamu na teknolojia za kisiasa zinazochochea ufanisi kwenye utendaji.
Rais Dk. Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali inaendelea na Ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani kwa kuifanya kuwa yenye uwezo wa kuhudumia meli nyingi zaidi ikwemo kampuni za kimataifa kuleta meli za mafuta kwenye bandari hiyo.