RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi ameweka jiwe la msingi la jengo la Taaluma na Utawala awamu ya pili katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS) ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam iliyopo Buyu visiwani Zanzibar.
Ujenzi wa jengo hilo ni miongoni mwa shughuli za utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaotekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu wa Benki ya Dunia kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo Januari 5,2025 visiwani humo, Rais Dkt. Mwinyi amefurahishwa na hatua iliyofikiwa ya ujenzi huo na wanatarajia kazi hiyo itakamilika kama ambavyo mkandarasi ameahidi na kwa mujibu wa mkataba uliosainiwa
“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa taasisi hii kwani ni taasisi muhimu na ina mchango mkubwa katika mipango yetu, na sera za Serikali ninayoiongoza katika kuendeleza uchumi wa buluu unaozingatia matumizi endelevu ya rasilimali za bahari”. Amesema
Aidha Dkt. Mwinyi amesema kupitia Chuo hicho watapata wataalamu wa uvuvi na wataalamu wa wanaojihusisha na masuala ya bahari kwa ujumla wake.
“Ninafuraha leo tumefikia hatua hii ya kuweka jiwe la msingi ili Chuo hiki kiwe kikubwa zaidi, kiwe bora zaidi na kuweza kutoa taaluma nyingi zaidi kwaajili ya kutunufaisha sisi hapa Zanzibar lakini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla wake.
Amesema matarajio yao makubwa ya Chuo hicho ni kuona kinawapatia matokeo ya tafiti mbalimbali zinazofanywa na zinazohusiana na uchumi wa buluu.
Pamoja na hayo amesema kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi wamepata mafanikio makubwa ya Maendeleo katika kila sekta ikiwemo sekta ya elimu .
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam ambaye pia ni Rais Mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete amemshukuru Rais Mwinyi kwa uwamuzi wake kuwawezesha kupata Hatimiliki ya Ardhi ya eneo hili la Taasisi ya Sayansi za Bahari.
Pia amemshukuru kwa kukubali maombi yao ya kutengenezewa barabara inayokuja hapo chuoni ambayo haikuwa katika hali nzuri.
“Wote ni mashuhuda kwa muda mfupi tu baadaye ahadi yako ya kuiboresha barabara ya kuja Buyu imetimia, tena imewekwa lami! kwa kweli hatuna budi kusema asante sana. Changamoto ya barabara haipo tena, na imerahisisha sana usafiri wa wanafunzi wetu ambao mabweni yao yapo Mazizini. Hivi sasa, mabasi ya Chuo yanachukua muda mfupi zaidi kufika hapa kuwaleta wanafunzi na wafanyakazi”. Amesema Dkt. Kikwete.
Pamoja na hayo ameishukuru Benki ya Dunia kwa ufadhili, Wamewapatia uwezo wa kukamilisha ujenzi wa Jengo la Taaluma na Utawala katika Taasisi hiyo. Kwa fedha walizopata pia watajenga Bweni moja la wanafunzi.
“Tunapendezwa sana na ushirikiano waliotuonesha ndugu zetu wa Benki ya Dunia. Katika hatua za utekelezaji wa mradi huu tumekuwa nao, na hata leo wawakilishi wao wameungana nasi kushuhudia uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi hapa Buyu”. Ameeleza
Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia Mhe.Prof Adolf Mkenda amesema mkopo wa bilioni 972 kutoka benki ya dunia ni kwaajili ya kuimarisha elimu vyuo vikuu nchini.
Nae Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amesema hatua ya ujenzi imefikia asilimia 50 na tayari mkandarasi ameshalipwa Shilingi Bilioni 4.2 ambayo inajumuisha majengo yote mawili.
Vilevile, amesema Mradi umetenga bajeti ya vifaa vya maabara kwa ajili ya vyumba vyote vya maabara na hatua za awali za ununuzi wa vifaa hivyo zimeanza kwa kuzingatia hatua ya ujenzi ulipofikia.Amesema Jengo la taaluma na utawala lina maabara tano, madarasa yatakayochukua wanafunzi 250, ukumbi wa kisasa wa mikutano utakaochukua watu 150 na ofisi za wafanyakazi.