Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema Jeshi la Polisi ni miongoni mwa taasisi za utoaji haki nchini ambayo inanyooshewa sana vidole, kulalamikiwa na wananchi juu ya rushwa kwa kupindisha haki na kuchepusha sheria.
Amesema watu 70 kati ya 100 utakaozungumza nao nchini wanalilalamikia jeshi la polisi kwa namna linavyofanya kazi huku akibainisha watu wasio na nyadhifa ama fedha wanapata tabu kupata haki zao.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Januari 31, 2023 Ikulu, Chamwino jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini.
Amesema Tume hiyo imepewa miezi minne kuanzia kesho hadi Mei 30 kukamilisha kazi hiyo na kukabidhi ripoti.
Amesema kwa kipindi cha miongo kadhaa mfumo haki jinai umekuwa na changamoto nyingi hivyo Serikali imeamua kuunda tume hiyo kutathmini mfumo wa utoaji haki na kimaadili katika taasisi hizo ili kubaini upungufu uliopo na kuja na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha utoaji haki nchini, huku akizitaka taasisi hizo kutoa ushirikiano wa kutosha ili tume ifanye kazi yake.
“Tukaliangalie jeshi la polisi ambalo mara nyingi kama utazungumza na watu 100 basi 70 watalinyooshea kidole,” Rais Samia
“Pia, ofisi ya mashtaka tuangalie kwenyewe kukoje na kuna kasoro zipi kuna nini haswa kilichoharibu hii taasisi. Tuiangalie Takukuru kwa sababu kubadilisha tu mkuu wa taasisi haisaidii watamdanganya tu wafanye wanavyotaka,” Rais Samia
“Jeshi la magereza na kwenyewe tukalitazame magereza zetu zikoje na zinatakiwa ziweje, mwendelezo wa magereza ukoje, inafanya kazi ya msingi? mamlaka ya kuzuia dawa za kulevya kuna malalamiko mengi tukaangalie kwa nini wanafanya hivyo suala la uzalendo liko wapi.” Rais Samia
“Mimi na nyinyi tunasimamia haki za watu hakuna kitu kibaya kama kuchepusha haki ya mtu twendeni tukaangalie tumeteteleka wapi ili tukalinde haki za watu,” Rais Samia