Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na kuzungumza nao kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kukuza biashara na uwekezaji hapa nchini pamoja na kupanua uwigo wa kodi.
Mkutano huo umefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo viongozi hao wamemshukuru Rais Samia kwa hatua alizoanza kuchukua kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa TPSF Angelina Ngalula amesema sekta binafsi imeanza kuona matokeo ya juhudi za Rais Samia ambapo kufuatia ziara ya nchini Kenya, sekta binafsi ya Kenya na sekta binafsi ya Tanzania wamekubaliana kuanzisha soko la pamoja la bidhaa ambalo litawawezesha wafanyabiashara wa pande zote kuuza na kununua bidhaa sokoni hapo na pia mpango wa bajeti ya mwaka 2021/22 umezingatia maoni ya sekta binafsi.
Hata hivyo, viongozi hao wameomba Serikali kuendelea kutilia mkazo juhudi za kuboresha zaidi mazingira ya kufanya biashara (Blue Print), kusimamia ulipaji wa kodi, kusimamia manufaa ya ndani (local content) katika miradi mikubwa, kufanya utafiti, kuvutia mitaji, uwekezaji katika maeneo ya kimkakati na kutilia mkazo kuendeleza kilimo ambacho kinaajiri Watanzania wengi.
Viongozi hao wamemuahidi Rais Samia kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanakuza zaidi uzalishaji kupitia sekta mbalimbali ili kukuza uchumi wa nchi, kuzalisha ajira na kuinua ustawi wa jamii.
Kwa upande wake Rais Samia amewapongeza viongozi hao kwa juhudi kubwa zinazofanywa na TPSF kuitikia wito wake wa kutekeleza jukumu la kukuza uchumi na amewahakikishia kuwa Serikali itawaunga mkono katika juhudi hizo.
Rais Samia ameahidi kufanyia kazi maoni yao pamoja na maoni mengine yatakayotolewa katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) unaotarajiwa kufanyika Juni, 2021.