Rais Samia Suluhu Hassan Jumatatu alithibitisha uwepo wa mlipuko hatari wa virusi vya Marburg kaskazini magharibi mwa nchi, huku kesi nyingine moja ya ugonjwa huo ikiripotiwa.
“Vipimo vya maabara vilivyofanyika katika maabara ya huko Kagera na baadaye kuthibitishwa jijini Dar Es Salaam, vilibaini mgonjwa mmoja alikuwa na virusi vya Marburg,” alisema katika mkutano na baadhi ya maafisa wa serikali na wizara ya afya ambao ulihudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya duniani (WHO) Tedros Adhanom Ghebreyesus mjini Dodoma.
Wiki iliyopita, waziri wa afya alikanusha kuwepo kwa mlipuko huo katika taifa hilo la Afrika Mashariki akisema hakuna mtu yeyote aliyeambukizwa virusi hivyo.
Ilikuwa baada ya WHO kusema kwamba ilipokea ripoti za kuaminika kwamba watu wanane walifariki kutokana na virusi vinavyoshukiwa kuwa Marburg katika eneo hilo hilo tarehe 10 Januari.