Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango wameipongeza Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushiriki kikamilifu kwenye Tamasha la Kizimkazi Zanzibar kwa kuandaa matukio kadhaa yanayochochea ukuaji wa kimichezo, burudani na utalii mwishoni mwa wiki Visiwani humo.
Katika matukio ya michezo benki hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) waliandaa tamasha kubwa la muziki lijulikanalo kama “Bongo and Zenji flavour night” lililofanyika Paje likihusisha uwepo wa Rais Samia.
Tukio hilo lilitanguliwa na mechi ya fainali ya ligi ya soka ya Vijana wa Kizimkazi ijulikanayo kama “Samia Kizimkazi Youth Cup” iliyofanyika Uwanja wa New Amaan Complex iliyoongozwa na Makamu wa Rais, Dk. Mpango.
Fainali hiyo ilihitimishwa kwa timu ya Shule ya Sekondari Kusini kuibuka mabingwa wa kombe hilo baada ya kuifunga Shule ya Sekondari Muyuni jumla ya magoli 3-0.
Katika kukabidhi zawadi kwa mabingwa hao vijana, ilishuhudiwa Makamu wa Rais, Dk. Mpango akiwaongoza wadau wengine wakiwemo viongozi waandamizi wa serikali pamoja na wadhamini wa ligi hiyo kampuni ya Mawasiliano TTCL na benki ya NBC walioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi.
Akizungumzia matukio hayo wakati wa uzinduzi wa mradi wa utalii wa Samaki aina ya Kasa uliopo kwenye Pango la Salaam (Salaam Cave) katika Shehia ya Kizimkazi Mkunguni uliodhamininiwa pia na benki ya NBC kwa ushirikiano na TTCL, Rais Samia pamoja na kuwapongeza wadau hao alionyesha kuguswa na jitihada zao katika kufanikisha tamasha hilo tangu lilipozinduliwa miaka 9 iliyopita.
“Pamoja na jitihada za wadau wengine wengi katika kufanikisha tamasha hili na kwa kuwa siku ya leo ni maalum kwa ajili ya NBC na TTCL nitumie fursa hii kuwashukuru sana na kuwapongeza kwa jitihada zao katika kufanikisha tamasha hili tangu lilipoanzishwa.
“Pamoja na jitihada nyingine nyingi leo hii wadau hawa wawili wametuandalia matukio makubwa matatu muhimu katika kufanikisha tamasha hili ukiwemo uzinduzi huu wa utalii wa kasa hapa Kizimkazi.
“Pamoja na hili pia wametuandalia mashindano ya mpira kwa vijana na zaidi pia leo wameratibu tamasha kubwa la burudani huko Paje…naahidi kushiriki,’’ alisema Rais Samia kabla ya kushiriki tamasha hilo baadae jioni.
Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi alisema tangu kuanzishwa kwa tamasha hilo miaka tisa iliyopita benki ya NBC imekuwa ikitumia vema fursa hiyo si tu kuandaa matukio ya michezo na burudani bali pia kufanikisha jitihada zake mbalimbali za kusaidia jamii hususani katika nyanja za elimu, afya, utalii, michezo na hata huduma za kifedha.
“Tangu kuanza kwa tamasha hili, tulianza kwa kushiriki ujenzi wa madarasa, baadaye tukatoa msaada wa gari la wagonjwa yaani NBC Mobile Clinic ambalo linaendelea kutoa huduma bora za afya, kisha tukashiriki ujenzi na ununuzi wa samani za Saccos ya Kizimkazi.
“Baadaae tuliendelea kushiriki ujenzi wa Kituo cha Afya na maeneo mengine ya muhimu ya maendeleo kwa wana-Kizimkazi.
“Kifupi, naweza kusema kuwa “sisi Benki ya NBC tumekuwa pamoja na wana-Kizimkazi toka wakati wakisema ‘kizimkazi inakuita’ mpaka leo mwaka 2024 tunaposema “Kizimkazi imeitika”. Aliongeza.
Akizungumzia ushiriki wa benki ya NBC kwenye uzinduzi wa Pango la Salaam (Salaam Cave), Sabi alisema benki hiyo ina nia thabiti ya kukuza utalii nchini na mfanikio ya mradi huo yatasaidia kuzalisha ajira na kuongeza pato la taifa kupitia utalii.
“Benki ya NBC tumejipanga ili kuweka mfumo wa maalum wa malipo ya kidijitali ili kurahisisha malipo ya watalii kwenye pango hilo na maeneo mengine kama haya hapa visiwani Zanzibar,’’ alibainisha