Rais wa Senegal Macky Sall ametangaza Jumatatu kuwa siku ya mapumziko kusherehekea ushindi wa timu ya taifa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon).
Rais ambaye alikuwa nje ya nchi amefutilia mbali awamu ya mwisho ya safari yake ili kuwakaribisha nyota hao wa soka kurejea nchini siku ya Jumatatu.
Rais Sall ataitunuku timu hiyo Jumanne katika ikulu ya rais, televisheni ya RTS ilisema.
Senegal ilishinda fainali ya kwanza ya Afcon baada ya kushindwa mara mbili katika fainali mwaka 2002 na 2019.
Waliishinda Misri 4-2 kwa mikwaju ya penalti na kupata ushindi wao baada ya fainali kumalizika bila bao kufuatia muda wa nyongeza.
Wakati huo huo, raia wameendelea kusherehekea usiku kucha kuamkia Jumatatu katika miji mbalimbali nchini Senegal kufuatia ushindia wa Kombe la Mataifa ya Afrika.
Video zinaonesha mashabiki wa timu hiyo wakiwa wanapeperusha bendera ya taifa hilo wakiwa wanacheza densi pamoja na ujumbe kutoka kila pembe uliokuwa unamiminika kwenye mitandao ya kijamii.