Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva atafanyiwa upasuaji wa nyonga siku ya Ijumaa na atafanya kazi kutoka kwa makao ya rais kwa takriban wiki tatu, maafisa walisema.
Wasemaji wa urais wa taifa hilo walisema Jumatatu kwamba kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto mwenye umri wa miaka 77 hataweza kusafiri kwa hadi wiki sita baada ya utaratibu huo. Lula amehisi maumivu ya nyonga tangu Agosti 2022.
Lula atafanyiwa upasuaji huo katika hospitali moja katika mji mkuu wa Brasilia.
Tangu mwanzoni mwa wiki amekuwa akivaa mask kuepusha magonjwa yatokanayo na hewa yanayoweza kusababisha kuahirishwa kwa upasuaji huo.
Lula anatarajiwa kusalia hospitalini hadi Jumanne wiki ijayo.
Mapema mwezi huu, Lula aliwaambia wafuasi wake wakati wa hafla ya serikali kwamba hakutaka kufanyiwa upasuaji huo wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka jana.
Alimshinda kwa taabu Jair Bolsonaro, katika uchaguzi wa Oktoba na akarejea miezi miwili baadaye kwenye wadhifa huo aliokuwa nao hapo awali 2003-2010.