Hotuba ya Rais wa Colombia, Gustavo Petro, imegonga vichwa vingi vya habari baada ya kusema biashara ya kokeini inaweza kudhibitiwa kwa urahisi ikiwa dawa hiyo itahalalishwa duniani kote, kwakuwa dawa hiyo si mbaya zaidi kuliko mvinyo aina ya whisky.
Katika mkutano wa mawaziri uliorushwa moja kwa moja, Petro amesema Kokeini ni haramu kwa sababu inatengenezwa , si kwa sababu ni mbaya zaidi kuliko whisky, japo bado wanasayansi wanachambua suala hilo.
Katika hotuba yake katika mkutano huo, Petro alipendekeza kuwa kokeini inapaswa kuhalalishwa kama vile pombe ili kukabiliana na biashara hiyo.
“Ikiwa unataka amani, lazima usambaratishe biashara (ya ulanguzi wa dawa za kulevya),” alisema. “Inaweza kusambaratishwa kwa urahisi ikiwa watahalalisha kokeini ulimwenguni. Ingeuzwa kama divai.”
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), kilimo cha majani ya coca nchini Colombia kiliongezeka kwa asilimia 10 mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku uzalishaji wa kokeini ukifikia tani zaidi ya 2,600, ongezeko la asilimia 53.
Colombia ni mzalishaji mkuu wa kokeini duniani, hasa kwa soko la Marekani na Ulaya, na serikali imekuwa ikipambana na biashara ya dawa za kulevya kwa miongo kadhaa.
Maoni yake yanakuja takriban wiki mbili baada ya mzozo wa kidiplomasia na Rais Donald Trump baada ya kuzuia kutua kwa ndege mbili za jeshi la Merika za wahamiaji waliofukuzwa, akiishutumu Amerika kwa kuwatendea wahamiaji wa Colombia kama wahalifu.
Baadaye Colombia ilikubali kuwapokea waliofukuzwa na kupeleka ndege zake kusaidia kuwarejesha, baada ya vitisho vingi vilivyojumuisha ushuru mkubwa, marufuku ya kusafiri kwa raia wa Colombia na kufutwa kwa viza kwa maafisa wa Colombia huko Marekani
Kiongozi huyo aliyeingia madarakani mwaka 2022, ameahidi kupambana na biashara ya dawa za kulevya na kudhibiti matumizi ya dawa haramu. Hata hivyo, tangu aingie madarakani, uzalishaji wa kokeini nchini Colombia umeongezeka.