Rais Ebrahim Raisi wa Iran amewasili Pretoria, mji mkuu wa kiutawala wa Afrika Kusini, alikoenda kushiriki mkutano wa kilele wa Jumuiya ya BRICS.
Ameandamana na ujumbe wa maafisa wa ngazi za juu wa Iran, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu, Hossein Amir-Abdollahian, Naibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Mohammad Jamshidi, na Mohammad Mokhber, Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hii.
Kabla ya kuondoka nchini kuelekea Afrika Kusini, Rais Raisi alisema jumuiya hiyo ni nguvu mpya inayoinukia kwa kasi duniani, na ambayo imefanikiwa kuyaleta pamoja mataifa huru yanayotaka kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na kukabiliana na ubeberu.
Aidha Rais Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu ina azma ya kuimarisha ushirikiano na BRICS ambayo inaundwa na nchi za Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini.
Mkutano huo wa jumuuiya ya nchi tano za BRICS pamoja na wakuu wa mataifa mengine yaliyoomba kujiunga na jumuiya hiyo ulianza mjini Johannesburg, Afrika Kusini juzi Jumanne, na unatazamiwa kumalizika leo.
Sayyid Raisi anatazamiwa pia kufanya mazungumzo na maafisa wa nchi zinazoshiriki mkutano huo mjini Johannesburg, kwa shabaha ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na pande kadhaa na nchi zinazoshiriki mkutano huo.
Hii ni safari ya 18 ya Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi, tangu achukue hatamu za uongozi mwezi Agosti mwaka 2021.