Rais wa Kenya William Ruto amemteua Jenerali Charles Muriu Kahariri kuwa Mkuu mpya wa Majeshi ya Ulinzi baada ya wadhifa huo kuachwa wazi kufuatia kifo cha Jenerali Francis Ogolla katika ajali ya helikopta.
Jenerali Kahariri alikuwa kamanda wa vikosi vya wanamaji na alipandishwa cheo kutoka Luteni Jenerali hadi cheo cha Jenerali kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu mpya wa kijeshi, wizara ya ulinzi ilisema.
Mtangulizi wake Jenerali Ogolla alikuwa miongoni mwa watu 12 waliokuwa ndani ya ndege ya kijeshi iliyoanguka muda mfupi baada ya kupaa kaskazini magharibi mwa Kenya mnamo Aprili 18. Watu wawili walionusurika wanaendelea na matibabu hospitalini.
Ajali hiyo inachunguzwa. Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa mkuu wa jeshi la Kenya kufariki akiwa ofisini.
Hapo awali Kahariri alikuwa naibu wa Ogolla.
Katika uteuzi mpya wa kijeshi, Rais Ruto alimtaja Meja Jenerali Fatuma Gaiti Ahmed kama kamanda wa Jeshi la Wanahewa la Kenya, mwanamke wa kwanza katika historia ya taifa hilo kushikilia wadhifa huo.
Anachukua nafasi ya John Mugaravai Omenda aliyepandishwa cheo na kuwa Makamu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na cheo cha Luteni Jenerali.