Rais wa Kenya William Ruto Jumatano alifanya mabadiliko katika baraza lake la mawaziri, kuongeza wizara mpya, na kuwateua maafisa wapya kuchukua nyadhifa mbalimbali serikalini.
Mawaziri 8 ni kati ya waliohamishiwa kwa wizara nyingine huku majukumu ya Waziri Mkuu Musalia Mudavadi yakiongezwa, na idara moja kuondolewa kutoka kwa afisi yake.
Rais Ruto pia aliwateua makatibu wakuu kadhaa, mabalozi na manaibu wao, huku akiwahamisha wengine kuhudumu katika wizara au balozi mbalimbali.
Rais huyo alifanyia mabadiliko baadhi ya wizara, huku idara mbalimbali zikihamishwa.
Mudavadi aliteuliwa kama Waziri wa mambo ya Nje na masuala ya Diaspora, na wizara hiyo kuhamishwa na kuwa chini ya afisi yake, ambayo ilibuniwa baada ya uchaguzi wa mwaka jana.
Mabadiliko hayo yalifanyika kufuatia ukosoaji wa utendakazi wa baadhi ya maafisa waandamizi wa serikali ya muungano wa Kenya Kwanza.
Mwezi Mei, Ruto alikiri kwamba baadhi ya mawaziri walikuwa wamezembea na kuonya kuwa iwapo hawangejirekebisha, wangechukuliwa hatua.
Mabadiliko hayo yalikuwa muhimu, Ruto alisema, “kuboresha utendakazi na kuimarisha utoaji huduma kama ilivyoainishwa katika manifesto ya utawala”.
Ruto amekabiliwa na msururu wa maandamano nchini kote kulalamikia gharama ya juu ya maisha na ongezeko la kodi tangu achukue mamlaka mnamo Agosti 2022.
Ni mara ya kwanza kwa Ruto kufanya mabadiliko kama hayo tangu aingie madarakani zaidi ya mwaka mmoja uliopita.