Rais wa Nigeria Bola Tinubu ametoa wito wa kusuluhishwa mara moja kwa kutokubaliana na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kulikoathiri safari za ndege na utoaji wa viza.
Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka jana uliacha kutoa viza kwa Wanigeria kufuatia kusimamishwa kwa safari za ndege na shirika la ndege la Emirates baada ya kushindwa kurejesha fedha kutoka nchi hiyo ya Afrika Magharibi kutokana na vikwazo vya malipo ya fedha.
Emirates ilisema wakati huo imeshindwa kupiga hatua baada ya “kufanya juhudi kubwa kuanzisha mazungumzo na mamlaka husika” kutafuta suluhu inayoweza kutekelezwa.
Siku ya Alhamisi, rais alisema suala hilo linafaa kutatuliwa “mara moja” akibainisha kuwa yuko tayari” kibinafsi” kuingilia kati suala hilo.
“Tunapaswa kuangalia masuala kama tatizo la kifamilia, na kulitatua kwa amani… Ni lazima tufanye kazi pamoja. Tunahitaji kukubaliana kuhusu masuala ya msingi ya usafiri wa anga na uhamiaji,” alisema. Alizungumza alipokuwa akimpokea balozi wa UAE, Salem Saeed Al-Shamsi, katika ikulu ya serikali katika mji mkuu, Abuja.
Bw Al-Shamsi alisema amekuwa akifanyia kazi mikataba 24 na serikali ya Nigeria na kuongeza kuwa “haya ni masuala madogo, na yatatatuliwa”.