Rais wa Falme za Kiarabu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan amewasamehe raia 57 wa Bangladesh waliopatikana na hatia mwezi Julai baada ya kufanya maandamano, shirika la habari la UAE WAM liliripoti Jumanne.
Sheikh Mohamed bin Zayed “ameamuru msamaha kwa raia wa Bangladesh waliohusika katika maandamano na ghasia za mwezi uliopita katika mataifa kadhaa,” ilisema taarifa hiyo.
“Uamuzi huo ni pamoja na kufuta hukumu za wale waliopatikana na hatia na kupanga kuwafukuza nchini.”
Mwanasheria mkuu wa UAE ametoa agizo la kusitisha utekelezaji wa hukumu na kuanza taratibu za kuwafukuza nchini, WAM ilisema.
Mwanasheria mkuu pia alitoa wito kwa wakaazi wote wa UAE kuheshimu sheria za nchi, akisisitiza kwamba haki ya kutoa maoni inalindwa na serikali na mfumo wake wa kisheria.
Raia hao wa Bangladesh walipatikana na hatia kwa kushiriki maandamano ya kuunga mkono maandamano yaliyoongozwa na wanafunzi nchini Bangladesh yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu Sheikh Hasina.
Mwezi Julai, mahakama ya Imarati iliwahukumu raia watatu wa Bangladesh kifungo cha maisha jela, wengine 53 kifungo cha miaka 10 jela na mmoja hadi miaka 11.