Rais wa Urusi Vladimir Putin ameeleza nia yake ya kuzuru Pyongyang hivi karibuni, shirika rasmi la habari la Korea Kaskazini KCNA limeripoti Jumapili.
Vladimir Putin amemshukuru kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un kwa mwaliko wake wakati wa mkutano wake na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea Kaskazini Choe Son Hui, ambaye alizuru Urusi wiki iliyopita, KCNA imesema, ikitoa mfano wa kuwajibika kwa Wizara ya Mashauri ya Kigeni. Urusi pia ilmeshukuru Korea Kaskazini kwa msaada na mshikamano wake katika vita vya Ukraine.
Nchi hizo mbili pia zimeonyesha wasiwasi mkubwa juu ya chokochoko za Marekani na washirika wake dhidi ya haki ya kujitawala ya Korea Kaskazini, na kukubaliana kushirikiana katika masuala ya kikanda, KCNA imesema. Ushirikiano huu lazima ufanyike kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Mataifa na sheria nyingine za kimataifa, imeelezwa.
Kwa upande wake, mwanadiplomasia mkuu wa Korea Kaskazini alisema nchi yake iko tayari kumpokea Rais wa Urusi Vladimir Putin. Maafisa wakuu wa Urusi, wakiwemo mawaziri wa ulinzi na mambo ya nje, waliitembelea Korea Kaskazini mwaka 2023, na hivyo kuzusha hofu ya uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya silaha.