Rais wa zamani wa Ivory Coast Laurent Gbagbo amekubali kupeperusha bendera ya chama chake kama mgombea urais katika uchaguzi wa 2025.
Katinan Kone, msemaji wa chama chake cha African People’s Party – Cote d’Ivoire (PPA-CI), ambacho Gbagbo alikianzisha mwaka 2021 alitoa habari hiyo baada ya mkutano wa kamati kuu ya chama hicho Jumamosi.
Akiwa ameachiliwa huru mwaka 2019 na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa mashtaka yanayohusiana na jukumu lake katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababishwa na kukataa kwake kukubali kushindwa katika uchaguzi wa 2010, Gbagbo alirejea Ivory Coast mwaka 2021.
Alipoteza udhibiti wa chama alichoanzisha hapo awali, Ivorian Popular Front (IPF), wakati amefungwa akisubiri kesi nchini Uholanzi kwa miaka kadhaa, lakini anaaminika kuwa bado ana wafuasi wengi na waaminifu nyumbani.
Uchaguzi ujao wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi unatarajiwa kufanyika Oktoba 2025. Rais Alassane Ouattara, 82, ambaye alichaguliwa tena mwaka 2020 bado hajasema iwapo atagombea tena.