Rais wa Zambia Hakainde Hichilema amewasamehe wafungwa 588 katika vituo mbalimbali vya kurekebisha tabia nchini humo.
Wafungwa walioachiliwa huru ni pamoja na wazee 11 na mama mmoja aliye na mtoto mchanga, kulingana na Waziri wa Mambo ya Ndani na Usalama wa Ndani Jack Mwiimb.
Mwimb siku ya Jumapili aliwaambia waandishi wa habari katika mji mkuu Lusaka, kifungo cha maisha jela kilibadilishwa hadi miaka 35 huku wafungwa wawili waliohukumiwa kunyongwa wakibadilishiwa kifungo cha maisha.
Kusamehewa kwa wafungwa hao na Rais Hichilema kuliendana na Ibara ya 97 ya Katiba ya nchi inayotoa mamlaka kwa rais kusamehe au kubadilisha adhabu zinazotolewa kwa watu waliotiwa hatiani.
Waziri huyo alisema wafungwa waliosamehewa wameonyesha tabia njema baada ya kufanyiwa taratibu za urekebishaji ambazo zitawawezesha kuunganishwa vyema katika jamii.
Uamuzi wa rais umepongezwa, haswa kutoka kwa mashirika ya kutetea haki za binadamu.