Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 imefanikiwa kuboresha hali ya maisha ya Mtanzania kwa kufanikisha utoaji bora wa huduma za kiafya kwa kusogeza huduma hizo kwa zaidi ya asilimia 78 kwa kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma za afya ndani ya kilomita tano kutokea kwenye makazi yake.
Rais Mwinyi ameyasema hayo alipokuwa akizindua Rasimu ya Kwanza ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Jumatano tarehe 11 Desemba 2024 Visiwani Zanzibar, ambapo ameeleza kuwa suala hilo limesaidia katika kupunguza idadi ya vifo nchini, kuongeza idadi ya wanawake wanaojifungua kwenye vituo vya afya pamoja na kuongeza wastani wa kuishi kwa Mtanzania kutoka miaka 52 mwaka 2000 hadi kufikia miaka sitini na tano na nusu mwaka 2022.
Aidha Rais Mwinyi amesema vifo vya uzazi kwa wanawake vimepungua kutoka vifo 750 kwa kila vizazi laki moja hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi laki moja kufikia mwaka 2022, huku pia vifo vya watoto wachanga vikipungua kutoka 85 mwaka 2000 hadi kufikia vifo 36 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa nchini Tanzania.
Akizungumzia maendeleo yaliyopigwa kwenye sekta ya elimu, Rais Mwinyi amesema kiwango cha wanaomaliza elimu ya msingi kimeongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 70 mwaka 2022 pamoja na kufanikiwa kuondoa pengo lililokuwepo kati ya wasichana na wavulana katika upataji wa elimu.