Kampuni ya Swissport Tanzania imeingia makubaliano ya kufanyakazi na Shirika la Ndege la Ufaransa na KLM katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo Tanzania, Mrisho Yassin maandalizi yamekamilika na timu yake imefanya kazi kubwa na anaamini huduma za kampuni ya Swissport zitafikia matarajio ya kampuni hiyo ya Ufaransa.
“Hatua hii ni muhimu sana kwa kampuni yetu ambayo historia inaonesha ilishawahi kufanya kazi na ndege za shirika la KLM miaka mitano iliyopita likaenda kwa washindani wetu. Tuna furaha leo wamerudi tena kwetu,” alisema Yassin.
Alisema pia safari hii KLM haiko yenyewe bali itakuwa na mshirika wake katika biashara ambaye ni Shirika la Ndege la Ufaransa hivyo kwa mara ya kwanza Swissport itafanyakazi na shirika hilo la Ufaransa.
“Tunaposherehekea kufanyakazi na Shirika la Ndege la Ufaransa, Dar es Salaam kitu hichohicho kinafanyika mkoani Kilimanjaro ambako operesheni za KLM zinaendelea,” alisema.