MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amezindua rasmi Tumaini Jema Group (TJG) linalohusisha mitaa minne ya Liwiti, Amani, Mfaume na Misewe lililopo Tarafa ya Ukonga Kata ya Liwiti Tabata Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.
Afisa Tawala Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Flora Mgonja akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kikundi hicho cha Kijamii iliyofanyika Februari 11, 2025 alisema ni cha muhimu sana kwani kimejikita zaidi kujiinua kiuchumi.
Alisema uanzishwaji wa kikundi hicho unaunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwainua kiuchumi ambaye anaangaika kutafuta fursa za kiuchumi ndani na nje ya nchi na kueleza kuwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam itaendelea kuwapa ushirikiano.
Mgonja aliwataka wanakikundi hicho kuchangangamkia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kwa wanawake, vijana, walemavu na makundi mengine hasa ikizingatiwa kuwa wana usajili wa Serikali.
Mgonja aliwapongeza wana kikundi hicho kwa kutunza hali ya usalama na utulivu nchini kwani bila ya amani hakuna kinachoweza kufanyika ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwezi Oktoba 2025 utakapo wadia wampe kura nyingi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Deogratias Kajula akizungumzia historia fupi ya kikundi hicho alisema wazo la kukianzisha liliibuliwa baada ya jirani yao mmoja kufariki na familia yake haikuwa na kipato cha kutosha kukidhi gharama za mazishi hivyo majirani walilazimika kushirikiana na familia kwa njia mbalimbali ili kuweza kumsitili marehemu.
Alisema wazo hilo liliweza kupata mashiko katika mitaa miwili ya Misewe na Liwiti ambapo wananchi wa mitaa hiyo walilipokea kwa mikono miwili na ndipo hatua za kutengeneza rasimu ya katiba ilipoanza.
Katibu wa Kikundi hicho, Stanley Mmanyi alisema malengo ya Tumaini Jema Group ni kushirikiana kijamii katika shida na raha, kushirikiana kiuchumi na kujiletea maendeleo akielezea suala la kusaidiana katika shida na raha ni kutembeleana na kujuliana hali hususan misiba na ugonjwa kwa mwanakikundi.
Akizungumzia kuhusu raha alisema ni kusaidiana na mwanakikundi iwapo atakuwa anaoa au kuolewa hama kuozesha na kuinuana kiuchumi kwa nia ya kujiletea maendeleo.
Mmanyi akitaja malengo mengine ya kikundi hicho kuwa ni pamoja na kuwekeza kwenye mifuko mbalimbali kama vile UTT-Amis, mabenki ya biashara, kukusanya maduhuli na tozo za Halmashauri mbalimbali zilizoko katika Mkoa wa Dar es Salaam kama vile kukusanya ushuru wa masoko, minada ya Halmashauri kwa makubaliano maalumu na halmashauri husika.