Mkuu wa Mkoa wa Iringa Halima Dendego amewataka Wafanyabiashara wadogo waliovamia eneo la ndani ya makaburi ya Mlandege ili kujenga vibanda vya biashara kuondoka mara moja kwani ni kinyume na maadili na kuiagiza Manispaa ya Iringa kujenga ukuta mara moja kuzunguka makaburi hayo.
RC Halima Dendego amesema hayo kwenye Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Iringa kilichofanyika leo ambapo amesema mchakato huo hauhitaji siasa huku akiahidi kuwaondoa wote waliovamia eneo hilo la ndani ya makaburi.
“Vijana wetu wameamua kuvamia makaburi ile hali imenisikitisha sana, jambo hili tuache siasa, halihitaji siasa tukemee ujinga wa namna hiyo na atakayeona ni halali Vijana wale wakae pale juu ya makaburi huyo atakuwa Adui yangu namba moja”
“Lile ni eneo takatifu wenzetu wamepumzika na sisi tutaenda kupumzika pale leo Watu wanapiga makofi kuona Vijana wale wamejenga kwenye makaburi, sio sawa ni kinyume na mila na desturi, hatutokubali jambo la kipuuzi kama lile, siasa hizi zisifanye tupoteze utu wetu mbele ya Mungu adhabu yake ni kali”
Ikumbukwe March 10,2023 ilikuwa siku ya mwisho ya Wamachinga kupanga vitu nje katikati ya Mji Wa Iringa na vibanda vyao vilibomolewa na kuambiwa wahamie Soko la Mlandege, hata hivyo baadhi ya Wamachinga wamesema kutokana na udogo wa Soko la Mlandege wamelazimika kulima eneo la makaburi na kujenga vibanda vyao.