Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Amos Makalla ameagiza kufunguliwa kwa Bar na Hotel zote zilizofungiwa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa kosa la kufungulia muziki mkubwa na kuweka utaratibu wa haraka wa kuelimisha makundi hayo.
Mhe. Makalla ametoa agizo hilo mapema leo ijumaa Mei 26, 2023 wakati wa kikao chake na wamiliki na wafanyabiashara wa Bar na hotel mkaoni humo kilichifanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
“Bar na hoteli hizi zikisimama, ajira zitasimama, biashara zitasimama na uchumi utasimama na tujiulize watawezaje kulipa faini wanazodaiwa wakati biashara wamefunga hawafanyi tena.” Amesisitiza Makalla.
RC Makalla amepiga pia marufuku ukamataji wa nguvu huku akibainisha kuwa wafanyabiashara hao sio majambazi hivyo wanapaswa kuelimishwa wanapokosea kwa kuangalia uhalisia wa maisha kwani kuua biashara ni rahisi sana kuliko kuijenga.
Aidha RC Makalla amewataka NEMC na wafanyabiashara waliopigwa faini kuketi pamoja na kuzungumza namna ya kumaliza matatizo hayo ili kuhakikisha biashara hazisimami kwa sasa na amewataka watulie na kuondoa hofu kutokana na tafrani za kamata kamata.
“Nataka NEMC watoke kwenye kuwa taasisi ya kamata kamata na kuwa kama chuo kwa kuwaona wadau wao kama watoto na wao kuwa walezi na wajikite kwenye kutoa elimu ili watambue nini wanapaswa kufanya na kitu gani hawapaswi kufanya.”–RC Makalla.
Akisoma risala kwa niaba ya wafanyabiashara hao, Richard Lomweti amesema operesheni inayofanywa na NEMC kwenye Bar na kumbi za starehe kuanzia Mwezi Mei 2023 imewaumiza kwa kuwapiga faini kubwa kwa kudai kuwa wanazalisha kelele tena bila kutoa elimu kwao hususani wakati wa kutoa leseni.
“Kifaa wanachotumia NEMC kinaonekana hakina uhalisia wa vipimo kwani hata muziki ukizimwa kinaonesha muziki umezidi kiwango na pia kinahusisha hata kelele zingine nje ya muziki husika kuwa ni kelele za muzuki.” Amesema bwana Lomweti.
Aidha, amefafanua kuwa faini wanazotozwa na NEMC pamoja na adhabu za kuwekwa ndani au kizuizini zimekuwa kubwa tofauti na uhalisia wa kosa hivyo wametoa wito kwa taasisi hiyo kuondoa faini hizo zinazowaumiza kiuchumi.
Vilevile, wameomba NEMC kuketi nao kwa pamoja kuzungumza na kuona namna ya kuboresha huduma hizo pasipo kubughuzi na kwamba wafute faini zote na kufuta sheria kandamizi zisizoendana na mazingira halisi ya uchumi wa sasa.