Balozi wa taifa la Urusi nchini Uturuki Andrey Karlov, ameuawa December 19 2016 kwa kupigwa risasi na mtu ambaye alikuwa nyuma yake. Imeelezwa kuwa aliyemshambulia ni afisa wa polisi ambaye hakuwa kwenye zamu wakati balozi huyo alipokuwa anatoa hotuba kwenye maonesho ya picha katika mji mkuu Ankara.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema kuuawa kwa balozi wa taifa lake nchini Uturuki ni uchokozi ambao lengo lake ni kuvuruga juhudi za kutafuta amani Syria. Kwa upande wa Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, amesema kuuawa kwa balozi huyo ni shambulio dhidi ya taifa la uturuki.
Picha za video zilimuonesha mshambuliaji, akiwa amevalia suti na tai, akimfyatulia risasi balozi huyo kutoka nyuma, akisema kwa sauti ujumbe kuhusu mji wa Aleppo, Syria, mshambuliaji huyo aliuawa kwa kupigwa risais na polisi.
Taarifa zinasema muuaji ni Mevlut Mert Aydintas ’22’, ambaye alikuwa anahudumu katika kikosi cha polisi cha kupambana na fujo mjini Ankara lakini haijabainika iwapo ana uhusiano wowote na kundi lolote.
Kisa hicho kilitokea siku moja baada ya maandamano kufanyika Uturuki kupinga hatua ya Urusi kumuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad. Recep Tayyip Erdogan alizungumza na Rais Putin kwa njia ya simu, na kwenye ujumbe wa video, alisema wote wawili walikubaliana kisa hicho kilikuwa “uchokozi”.
VIDEO: ‘Kwanini mpaka sasa kuna kesi 1 tu Mahakama ya Mafisadi’ – Dr. Mwakyembe, Bonyeza play hapa chini kutazama