Mchezo wa soka kwa hatua ilioufikia kwa sasa ni biashara kubwa sana ambayo inategemea uwekezaji mkubwa sana ili iweze kuendelea.
Pamoja na ukweli kuwa huu ni mchezo mwepesi ambao huhusisha wachezaji 22 wanaopambana uwanjani, ushindi husakwa kwa njia za kisasa kwa miaka ya hivi karibuni njia ambazo zinahusisha teknolojia ya hali ya juu ambayo kila siku inaboreshwa.
Klabu ya Real Madrid ni mfano wa hatua hii ambayo imefikiwa kwenye mchezo wa soka, makao makuu ya Real Madrid yanaakisi aina ya maendeleo ambayo klabu ya ukubwa wake inapaswa kuwa nayo.

Klabu hii inamiliki jingo kubwa la makao makuu ambalo ndani yake kuna kila kitu kuanzia viwanja vya kisasa mpaka vyumba vya kupumzikia wachezaji hasa wakati wakiwa kwenye maandalizi ya kuelekea mechi kubwa.
Ukiachilia mbali viwanja na vyumba bora vinavyowahakikishia wachezaji mapumziko mazuri , eneo hilo lina vyumba vya kupumzikia ambavyo vina mashine za michezo ya kompyuta maarufu kama Video Games au Playstation pamoja na michezo mingine kama basketball na volleyball.






