Rais Vladmir Putin hivi karibuni alisema kuwa katika mwaka 2023, Moscow imewaajiri kwa hiari wanajeshi 486,000 kwa ajili ya jeshi na kwamba juhudi za kuliimarisha jeshi hilo mwaka ujao zitaongezeka.
Huku hayo yakijiri kiongozi mwandamizi wa kijeshi wa Ujerumani alisema katika mahojiano yaliyochapishwa leo Ijumaa kwamba Russia imepata hasara kubwa ya kibinadamu na mali nchini Ukraine na jeshi lake litaibuka likiwa dhaifu kutokana na mzvita vinavyoendelea.
Mahojiano hayo yamejiri wakati Kyiv inapigania kudumisha msaada wa magharibi kwa vita vyake dhidi ya vikosi vya Russia, ambavyo vilivamia Ukraine kwa mara ya kwanza mwezi Februari mwaka 2022.
“Unajua kwamba kwa mujibu wa takwimu za kijasusi za nchi za Magharibi, wanajeshi 300,000 wa Russia wameuawa au kujeruhiwa vibaya kiasi kwamba hawawezi tena kushirikishwa kwa vita,” Christian Freuding, ambaye anasimamia shughuli za uungaji mkono wa jeshi la Ujerumani kwa Kyiv, aliliambia gazeti moja nchini mwake.
Taarifa za kijasusi za Marekani zilizovuja mapema mwezi huu zilionyesha kuwa wanajeshi 315,000 wa Russia wameuawa au kujeruhiwa nchini Ukraine tangu vita kuanza.
Hata hivyo, Russia inafanikiwa kuendelea kuajiri wanajeshi “ikiwa ni pamoja na kutumia wafungwa, Na, bila shaka, tunaona uwekezaji mkubwa katika sekta ya silaha “, Freuding alisema.