Rais William Ruto wa Kenya amekosolewa kwa kushindwa kutekeleza kivitendo agizo lake la kuwazuia maafisa wa serikali kushiriki michango ya harambee kama mojawapo ya njia za kupambana na ufisadi.
Rais Ruto alitoa agizo hilo Julai 2024 ili kuzima maandamano ya vijana wa Gen Z waliolalamika kuwa hulka ya viongozi na maafisa wakuu serikalini ya kutoa pesa nyingi katika michango hiyo inaendeleza uovu wa ufisadi.
Wakati huo, mbunge wa Kapseret, Oscar Sudi, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, alishutumiwa kwa kutoa Shilingi milioni 20, wakati mmoja, katika harambee, huku watu wakihoji chanzo cha pesa hizo.
Hata hivyo, Jumapili ya jana Septemba 15, 2024, saa chache baada ya kuwasili nchini akitoka ziarani nchini Ujerumani, Rais William Ruto wa Kenya pamoja na wandani wake walihudhuria ibada katika Kanisa la Stewards Revival Pentecostal, Nairobi ambako alijitolea kutoa mchango wa Sh. milioni 10 kusaidia ujenzi wa jengo jipya katika kanisa hilo.
Rais Ruto alijaribu kutetea hatua hiyo akidai kwamba kile alichofanya si harambee, bali ni “mchango tu”.
Alipokuwa akitangaza hatua ambazo serikali yake itachukua kuzuia maafisa wakuu na watumishi wa umma kushiriki michango ya harambee, Rais Ruto aliagiza Mwanasheria Mkuu kubuni sheria ya kufanikisha hatua hiyo.