Raia wa Rwanda wameendelea na maombolezo kufuatia vifo vya watu zaidi ya 130, waliofariki kutokana na mafuriko yaliyokumba eneo la magharibi mwa nchi hiyo, ambapo mamia ya nyumba zimeharibiwa.
Maombolezo haya yanafanyika wakati huu Serikali ikiendelea kukadiria hasara iliyotokana na mafuriko hayo, huku shughuli za mazishi pia zikiendelea katika moja ya majanga mabaya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo.
Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Rwanda, zilisababisha kutokea kwa maporomoko ya udongo yaliyoharibu nyumba na miundombinu mingine kama barabara, hasa katika eneo la magharibi mwa nchi linalopakana na ziwa Kivu ambako kumeripotiwa maafa zaidi.
Baadhi ya familia zimeeleza namna zilivyopoteza ndugu zao, baadhi kama Anonciata, anasema amepoteza mtoto wake baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo na kuta za nyumba yake na alifariki wakati akipatiwa matibabu hospitalini katika wilaya ya Karongi.
Aidha wengine mbali na kupoteza ndugu zao, wamesema shughuli za maisha ya kawaida zimekoma rasmi baada ya kupoteza mali nyingi ambazo walikuwa wakizitegemea kukimu familia zao.
Tangu Mei 2 maeneo ya kaskazini, magharibi na kusini mwa Rwanda, yameshuhudia mafuriko yaliyosababisha maafa kwa raia, huku miongoni mwa waliofariki wakiwemo wanafunzi 15 na shule 33 kuharibiwa.
Vifo vya wanafunzi viliripotiwa kwenye miji ya Karongi, Nyabihu, Ngororero na Rubavu, ambapo tayari baadhi wamezikwa huku shirika la msalaba mwekundu nchini humo likiendelea kuwasaidia waathirika.
Tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, wameanza kutoa misaada kwa raia walioathirika, ikiwemo makazi ya muda, chakula, dawa na mahitaji mengine muhimu.