Rwanda imefunga mitambo yake yote ya kuzalisha umeme kwa kutumia dizeli mwezi Juni mwaka huu, na kupanua uzalishaji wa umeme kwa nishati ya maji na gesi ya methane.
Akizungumza wikiendi kwenye mahojiano na wanahabari Waziri wa miundombinu wa Rwanda Bwana Jimmy Gasore, amesema mitambo miwili mipya ya kuzalisha umeme kwa nishati ya maji ya Rusumo na Shema ilifunguliwa hivi karibuni, hatua iliyowezesha kufungwa kwa mitambo ya kuzalisha umeme kwa dizeli.
Mradi wa kituo cha Rusumo ni mpango wa pamoja wa Rwanda, Burundi, na Tanzania, ambao baada ya kukamilika unatarajiwa kuzalisha 80MW, huku kila nchi ikipata 26.6MW.
Mradi wa kituo cha Shema ni mtambo wa kuzalisha umeme wa gesi ya methane ambao unalenga kuzalisha 56MW.
Kabla ya kufungwa kwa mitambo ya dizeli, Rwanda ilikuwa na mitambo mitano kama hiyo, na kuzalisha asilimia 26.76 ya jumla ya umeme nchini humo mbali na hayo, Rwanda pia ina mitambo minne ya kuzalisha umeme kwa kutumia nishati mbadala.
Kwa jumla, mitambo hiyo ilikuwa ikizalisha asilimia 51 ya jumla ya umeme nchini kabla ya kufungwa kwa mitambo ya dizeli.