Wizara ya Teknolojia na Ubunifu nchini Rwanda na washirika wake, mnamo Novemba 5, ilizindua rasmi maabara ya roboti katika shule ya New Generations Academy jijini Kigali.
Kulingana na tangazo liliotolewa na Rwanda TV, nchi hiyo imezindua maabara ya roboti yenye thamani ya faranga milioni 100 za Rwanda, kwa ajili ya kuboresha ilimu katika sekta ya teknolojia ya roboti.
Kati ya vifaa vyake ni vifaa vya sauti vya uhalisiai (virtual reality headsets) vinavyowawezesha wanafunzi kuingia katika mazingira ya mtandaoni ya 3-D, na droni zinazotoa fursa za mazoezi ya urubani na simulizi za kiutendaji.
Yves Iradukunda, Katibu Mkuu wa Wizara ya Teknolojia na Ubunifu, ameipongeza hatua ya serikali kuwekeza katika maabara hiyo na kusema, “Tunataka watoto waanze kutumia teknolojia hii na kuizoea. Roboti ni zana inayotumika sana ambayo inaweza kutumika katika tasnia, maisha ya kila siku, na kwingineko.
Hii inalingana na mpango wetu wa kuanzisha teknolojia kwa watoto wenye umri mdogo. Hapo awali, maonyesho kama haya yalikuwa yametengwa kwa vyuo vikuu, lakini sasa tunaifanya iweze kupatikana kwa wanafunzi wachanga, kuwasaidia kukuza ujuzi muhimu mapema”.
Naye Jean Claude Tuyisenge, Mkurugenzi Mtendaji wa shule hiyo, anaona maabara ya Roboti kama daraja la kuziba pengo la teknolojia iliyopo kati ya wanafunzi wadogo na kuboresha elimu katika sekta hiyo.
Vile vile Tusiyenge aliishukuru serikali ya Rwanda kwa kuwekeza katika mradi huo na kusema haitosaidia tu shule ya New Generation Academy, bali na shule zote jirani.
Kulingana na Tusiyenge, “Wanafunzi kutoka darasa la 1 hadi 7 tayari wanaonyesha ubunifu wa ajabu, na kuifanya maabara hii kuwa sehemu kuu ya elimu na maendeleo yao.”
Hadi sasa wanafunzi 25 na walimu watano hivi wanaweza kutumia maabara katika kipindi kimoja, na shule za Kigali pia zinaweza kuitumia wakati wa likizo au wakati wa programu za kawaida za shule.