Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda (FDA) imepiga marufuku dawa 22 za mitishamba ambazo hazikidhi viwango vya usalama na ubora. Uamuzi huo unafuatia matokeo ya vipimo vya kimaabara ambayo yamebainisha vipengele visivyo na viwango ndani ya bidhaa hizo.
Taarifa iliyosainiwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo Emile Bienvenu, inasema baada ya vipimo vya maabara kuonyesha bidhaa hizi zilizochanganuliwa hazikidhi viwango vinavyohitajika vya usalama na ubora, zinatakiwa kuondolewa sokoni.
Matokeo ya vipimo yameonesha kuwa bidhaa zote zilizoorodheshwa zinaweza kuleta madhara kwa afya ya binadamu.
FDA imeziagiza pande zote zinazohusika, ikiwa ni pamoja na watengenezaji, waagizaji, wauzaji wa jumla na rejareja, wasambazaji na watumiaji wanaohusishwa na bidhaa hizi, kusitisha usambazaji na matumizi kutokana na hatari zinazoweza kutokea kiafya.