Leo August 18, 2017 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imempa masharti ya dhamana Raia wa Afrika Kusini, Menelaos Tsampos anayekabiliwa na kesi ya kutishia kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa kompyuta.
Hakimu Mkazi Mfawidhi, Cyprian Mkeha ametoa masharti hayo wakati akitoa uamuzi dhidi ya pingamizi la upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa huyo asipewe dhamana akisema mshtakiwa huyo ana haki ya kupata dhamana hata kama ni raia wa kigeni.
Akitaja masharti ya dhamana, alisema mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Tsh. Milioni 20, awasilishe hati ya kusafiria na kuripoti kituo cha Polisi Kawe mara moja kwa wiki.
Baada ya kueleza hayo, Wakili wa utetezi Jebrah Kambole aliomba wapewe muda kwa ajili ya kutimiza masharti hayo ikiwemo kuwasilisha Passport ambapo kesi imeahirishwa hadi September 4, 2017.
Mshtakiwa huyo anakabiliwa na makosa manne likiwemo la kutishia kwa njia ya mtandao ambapo June 22, 2017 maeneo ya DSM kupitia mfumo wa Kompyuta alituma ujumbe wa E-mail uliokuwa na maneno ya vitisho kwa mtu anayeitwa Costa Gianna, ikiwa ni kinyume na sheria ya mtandao kifungu cha 23(1) na (2) namba 14 ya mwaka 2014.