Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) limezindua upya safari zake za ndege za kila siku kati ya Johannesburg na Dar es Salaam nchini Tanzania.
“Njia hii ya anga si tu hatua muhimu kwa SAA na kuunganisha Johannesburg na Dar es Salaam kupitia usafiri wa anga, bali pia inatangaza daraja linalounganisha mataifa mawili yenye ushawishi mkubwa kiuchumi barani Afrika na kuimarisha urafiki kati ya mataifa yetu,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa SAA, Profesa John Lamola.
“Inaleta pamoja viwanda, jumuiya na rasilimali, na kutuwezesha kufungua ustawi zaidi, kukuza ushirikiano na kuzalisha fursa mpya za biashara, uwekezaji na maendeleo kwa uchumi wetu, na kwa watu wa Afrika Kusini na Tanzania.”
Ukuaji mkubwa wa uchumiDar es Salaam ni jiji kubwa la Afrika Mashariki kwa idadi ya watu na ni kitovu muhimu cha kiuchumi na utaratibu wa ugavi na usafirishaji wa watu na mizigo kikanda. Pia ni lango la vivutio maarufu vya utalii katika ukanda huu.
Afrika Kusini inachangia sehemu kubwa ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni nchini Tanzania, na nchi hizi mbili zina biashara kubwa za mazao ya kilimo, madini ya thamani, kemikali na mashine.
Lamola anasema kwamba uzinduzi huu unawakilisha mpango mkakati wa SAA wa kuimarisha kuwepo kwa shirika hili barani Afrika.
“Mtandao wa kikanda wa SAA umeibuka kama mtendaji bora, na kuchangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Shirika la SAA. Muhimu zaidi, uhusiano huu wa kikanda ni muhimu kwa ukuaji mpana wa uchumi wa Afrika Kusini,” anasema.
Ratiba ya ndege
Ndege za kila siku zitaondoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa OR Tambo Jijini Johannesburg saa 4:00 usiku (SAST) na kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam saa 8:30 alfajiri (EAT). Ndege ya kila siku kutoka Dar es Salaam hadi Johannesburg itaondoka saa 11:10 alfajiri (EAT) na kuwasili Johannesburg saa 1:55 asubuhi (SAST). Dar es Salaam iko saa moja mbele ya Johannesburg.
Lamola anasema ratiba ya safari saba za ndege zinazorejea kila wiki imewekwa ili kuwahudumia abiria wanaowasili na wanaonganisha safari zao.
Kuunganisha mtandao wa kikanda wa SAA
Novemba mwaka jana, SAA ilipanua huduma zake za ndege hadi Harare (Zimbabwe) na Lusaka (Zambia) hadi safari 12 za ndege kwa wiki, kutoka safari 10 (Harare) na saba (Lusaka) kwa wiki. Safari za ndege kwenda Lagos (Nigeria) na Accra (Ghana) zimeongezwa kutoka mara tatu hadi nne kwa wiki, huku SAA ikisafiri hadi Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mara tano kwa wiki. SAA pia imeanza kuruka hadi kitovu cha uchimbaji madini cha DRC, Lubumbashi, Novemba.
Zaidi ya hayo, SAA imeongeza masafa ya safari zake za hadi Perth nchini Australia hadi safari tano za kila wiki kutoka Januari 7 mwaka huu.