Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetangaza siku 14 kwa watumiaji wa Vyombo vya Moto barabarani kuondoa namba za magari zilizoongezwa ukubwa maarufu kama (3D) na Vimulimuli kwa magari yote yasiyoruhusiwa kuwekwa, namba zote zenye vibao vyeusi na zizonatumia namba za chasis, taa zozote na stika ambazo zimeongezwa kwa matakwa ya wamiliki au madereva.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijimi dar es salaam, baada ya Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani leo Machi 04, 2024 Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Mhe. Jumanne Sagini (Mb) alisema kuwa namba hizo hazitengenezwi na wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), bali zinatengenezwa kiholela mtaani na herufi hizo kubandikwa juu ya namba halali na kutosomeka katika umbali unaotakiwa ambapo katika viwango vya TBS namba ya chombo cha moto isomeke kwa umbali usiopunga mita 100 ambapo 3D haifiki kiwango hicho.
“Mambo yote yanayohusiana na Usalama Barabarani hufanywa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa mtu mmoja mmoja au binafsi kwa mujibu wa usalama barabarani kuhusu matumizi ya namba yamebainishwa vizuri sana na sheria kwamba Namba zinazowekwa zinatakiwa ziweje? ziwe zimeandikwa na nani? anayetambulika na nani? ziwe na ubora gani? namba hizi zote hazijawekwa kwa bahati mbaya,” Alisema Sagini
Mhe. Sagini alisema kuwa, Ving’ora vinatoa ishara fulani ili magari mengine yaweza kupisha na hapa nisisitize kuwa, magari yanayotakiwa kuwekwa Ving’ora yanajulikana kama ya Polisi, Zimamoto ya Wagonjwa na yale yaliyopo katika misafara ya Viongozi kufanya hivyo bila kibali maalum ni ukiukwaji wa sheria.
Aidha, Naibu Waziri Sagini alisema kuwa, zoezi la ubanduaji wa namba zilizoongezwa ukubwa litaendeshwa hata kwenye magari ya Serikali ambapo yakibainika na makosa ya namna hiyo wanaotumia watachukuliwa hatua.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani Naibu Kamishna wa Polisi DCP Ramadhani Ng’anzi alisema kuwa, wanapiga marufuku namba zilizoongezeka ukubwa kwa sababu kiusalama Namba za 3D sio salama na namba za magari lazima ziwe 2D kutokana na mifumo na kamera kutotambua 3D.
“Baada ya Tarehe 15 Machi, 2024 tutaendelea kuzibandua na tukiona ile plate namba haisomeki vizuri tutakukamata na hili zoezi mnatakiwa muondoe wenyewe kwa hiyari lasivyo Jeshi la Polisi litakukamata kwa kuvunja sheria hata tukikuta namba haisomeki vizuri yaani imechubuka,” Alisema.
Aidha, Kamanda Ng’anzi aliongezea kuwa, Operesheni itajumuisha na Taa/Sport light kinyume na taratibu za mtengenezaji au kibali kutoka kwa Mkaguzi wa magari na uwekaji wa stika za rangi mbalimbali kwenye taa kubwa mbele na nyuma ya gari, ambazo zinabadilisha mwanga wa taa halisi mfano stika nyeusi, blue nyekundu na tinted.