Mkuu wa Shirikisho la Soka la Cameroon (Fecafoot) Samuel Eto’o amepigwa marufuku kuhudhuria mechi za timu ya taifa kwa muda wa miezi sita baada ya kukiuka kanuni za nidhamu za FIFA, bodi inayosimamia soka ilisema Jumatatu.
Mshambulizi huyo wa zamani wa Barcelona amekuwa rais wa Fecafoot tangu 2021 na sasa atapigwa marufuku kushiriki michezo yote ya wanaume na wanawake katika makundi mbalimbali ya umri.
“Adhabu hiyo iliwekwa kuhusiana na mechi ya hatua ya 16 ya Kombe la Dunia la FIFA kwa Wanawake U-20 kati ya Brazil na Cameroon iliyochezwa Bogota, Colombia, Septemba 11, 2024,” FIFA ilisema katika taarifa
Maelezo kuhusiana na matukio hayo hayakuwekwa wazi na kamati ya nidhamu ya FIFA.
Taarifa hiyo ilisema Eto’o alichukuliwa kuwa na hatia ya “tabia ya kuudhi na ukiukaji wa kanuni za mchezo wa haki,” pamoja na “utovu wa nidhamu” unaohusisha maafisa.
Marufuku hiyo inafuatia faini aliyotozwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 43 na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) chini ya miezi mitatu iliyopita, kutokana na uchunguzi kuhusu ukiukaji wa viwango vyake vya maadili na uadilifu.