Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewataka Watendaji wa Wizara ya Maji kutekeleza miradi kwa weledi, viwango na kuzingatia uadilifu.
Mhe. Aweso amesema hayo wakati akifungua Mkutano wa wadau wa Sekta ya Maji katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (wa AICC) Jijini Arusha, ambao unafanyika kwa siku mbili na kutaka Sekta Binafsi ipewe kipaumbele kama mdau mkuu katika kufanikisha masuala ya maji katika jamii.
Amewashukuru na kuwapongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es salaam (DAWASA), Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Geita (GEUWASA). Wote hao wamepongezwa kama sehemu ya usimamizi mzuri wa miradi ya maji kwa kutumia chini ya kiwango cha fedha zilizotakiwa kwenda kwa wakandarasi.
Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Maji, umeitishwa na Wizara ya Maji ukiwa na lengo la kuwashukuru wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji kwa mchango wao mkubwa katika kuwezesha mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Maji nchini, wakiwemo Wadau wa Maendeleo, AZAKI, Wakandarasi, Wazabuni, Sekta Binafsi ikiwamo kampuni za uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazotumika katika Sekta ya Maji na Wafadhili wengine.
Sambamba na hilo, wadau watapata fursa ya kujadili na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu Rasimu ya Sera ya Taifa ya Maji ya Mwaka 2002, Toleo la Mwaka 2023 na Mpango Mkakati wa Wizara.
Pamoja na masuala mengine ambayo Serikali inatakiwa kuyajua na kuyafanyia kazi katika Sekta ya Maji.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof. Jamal Katundu akizungumzia mkutano huo amesema maoni na mapendekezo ya wadau wa Sekta ya Maji ni muhimu sana katika kuandaa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, toleo la 2023 katika kutekeleza dhana ya ushikishwaji.
Mkutano wa wadau wa sekta ya maji, pamoja na wengine, umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwenyekiti wa Bodi ya Maji ya Taifa, Wenyeviti wa Bodi za Mabonde ya maji na wa Mamlaka za maji, RUWASA, Uongozi wa Chuo cha Maji, viongozi wa chama na serikali mkoa wa Arusha, Menejimenti ya Wizara ya Maji na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za maji wa Mikoa na Wilaya.