Sekta ya Afya kuendelea kuweka kipaumbele ajenda ya kupunguza vifo vya mama na mtoto katika vikao vinavyofanyika ngazi zote za Mkoa ili kuendelea kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi ikiwa ni malengo ya Taifa na Dunia.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule leo Januari 15, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi chenye lengo la kujadili mikakati ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, mama na watoto.
“Kupunguza vifo vya mama na mtoto ni malengo ya Dunia lakini pia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni dhamira yake hivyo sisi watendaji wake ni lazima tupambane nayo kwa kumuunga mkono Rais na Dunia kwa ujumla.” Amesema Mh. Senyamule.
Amesema, ni vyema Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Kijiji awe anashiriki vikao vya kikanuni katika ngazi zote za Halmashauri ili aweze kutoa taarifa ya hali ilivyo juu ya vifo vinavyotokea pamoja na changamoto zake.
“Kama kuna mama mjamzito ambae hafiki katika vituo vya kutolea huduma za Afya tupate taarifa ili watendaji wa Wilaya na Kijiji wazidi kutoa rai na kuelimisha kupitia mikutano yao ya hadhara kwa wananchi.” Amesema Mhe. Senyamule.
Aidha, Mhe. Senyamule ametoa wito kwa Waganga Wakuu wa Wilaya kupeleka taarifa za Wilaya juu ya vifo vya mama na mtoto kila wiki katika ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kuwa na mkakati wa pamoja wa kuondoa vifo visivyo na ulazima kwa kushirikiana na wataalamu.