Wagombea 15 kati ya 20 walioidhinishwa kugombea katika uchaguzi wa urais wa Senegal ambao uliakhirishwa kufanyika mwezi huu wa Februari wametaka uchaguzi huo mpya uwe umeshafanyika kabla ya tarehe Pili Aprili.
Rais Macky Sall, ambaye muhula wake unamalizika rasmi siku hiyo, alitangaza kuahirishwa uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25 saa chache kabla ya kampeni rasmi kuanza.
Hatua hiyo iliitumbukiza Senegal katika machafuko mabaya zaidi ya kisiasa kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa.
Wiki iliyopita, Baraza la Katiba ambalo ni chombo cha juu cha Katiba cha nchi hiyo kilibatilisha uamuzi huo wa Sall.
Hata hivyo, suali linabaki kama uchaguzi huo utafanyika kabla ya rais Sall kuondoka madarakani, na kama utashirikisha wagombea wale wale waliopitishwa hapo awali au la.
Wagombea 15 kati ya 20 waliopitishwa awali wametia saini barua iliyoonekana na AFP jana Jumatatu, ikisema, “tarehe mpya ya upigaji kura na tarehe ya makabidhiano madaraka kati ya rais na mrithi wake lazima iwe kabla ya Aprili Pili”.