Mafunzo ya waandishi wa habari wa Mitandaoni leo yapo siku ya pili hapa mkoani Iringa huku mada kuu ambayo imekuwa na mvuto ni uwepo wa sensa ya majengo katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itayofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa kutoa mafunzo hayo Mratibu wa Dodoso la Majengo kutoka Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Amina Ramadhani amesema kuwa Sensa hii inakwenda kutambua kila jengo lililopo juu ya uso wa ardhi ya Tanzania.
“Mwaka huu kupitia Sensa ya Watu na Makazi, tunakwenda kukusanya taarifa za majengo yote nchini, tunafanya hivyo kwa kuwa hatukuwahi kuwa na taarifa hizo. Na katika hilo tumeandaa Dodoso la maswali 25” Amesema Ramadhani.
Amina Amesema lengo la sensa ya watu na makazi ni kupata taharifa sahihi za kidemografia ,kijamii,kiuchumi na hali ya mazingira kwa lengo la kupata Takwimu sahihi zitakazowezesha serikali na wadau wengine kupanga kwa usahihi mipango ya maendeleo ya watu wake katika sekta mbalimbali.
Aidha mbali na kuelezwa umuhimu wa Sensa ya majengo pia wanahabari hao wamepata kufundishwa juu ya changamoto za kuripoti habari wakati wa zoezi la sensa.
Akizungumza wakati wa kutoa mada Dkt. Darius Mukiza, Mhadhiri, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari, Chuo Kikuu Dar es Salaam amesema
bila Sensa nchi haiwezi kuweka mipango yake ya maendeleo, haiwezi kujua idadi halisi ya watu wake, kupitia sensa pia huanisha mahitaji ya huduma za jamii zinazohitajika
Amesema kuwa Waandishi wa habari wa mitandao ya kijamii wanapaswa kuwaeleza wananchi kupitia majukwaa yao kuwa taarifa zitakazotolewa kwa Karani wa Sensa zitakuwa Siri na zitatumika kwa madhumuni ya kitwakimu peke yake katika kusaidia serikali kupanga maendeleo.