Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika michezo ya kubahatisha nchini kwa kuwa ni moja ya chanzo muhimu cha mapato ya kusaidia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), wakati wa hafla ya kutambulisha Kampuni ya ITHUBA kama mwendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa baada ya kuibuka mshindi katika mchakato wa zabuni ulioendeshwa na Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).
Mhe. Chande alisema kuwa, Serikali inajivunia hatua ilizochukua kufanikisha mradi huo mkubwa wa mabadiliko ya Bahati Nasibu ya Taifa ambayo ni ishara ya matumaini, fursa na maendeleo, ambapo kila tiketi ya Bahati Nasibu inayonunuliwa, mbali na nafasi ya kushinda, ni mchango kwa maendeleo ya Taifa letu.
Aliongeza kuwa uteuzi wa Kampuni ya ITHUBA Tanzania kama mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa unaonesha uwezo wao wa hali ya juu na uelewa wa kina wa mahitaji ya Tanzania na uteuzi huo ulizingatia utaalam na uzoefu wa ITHUBA, kama mwekezaji wa kimataifa mwenye rekodi nzuri ya kuendesha biashara ya Bahati Nasibu za Taifa barani Afrika ambako inaendesha michezo hiyo katika nchi ya Afrika ya Kusini, Uganda na nyinginezo.
“Ni imani yangu kuwa ITHUBA imejipanga vyema ili Bahati Nasibu ya Taifa iweze kuendeshwa kwa ufanisi na kuleta mafanikio yaliyotarajiwa na hatua hii inafungua matarajio makubwa katika ufanisi wa uendeshaji wa Bahati Nasibu ya Taifa na ukurasa mpya wa mabadiliko katika sekta ya michezo ya kubahatisha hapa nchini Tanzania” alisema Mhe. Chande.
Mhe. Chande alitoa wito kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), kuhakikisha wanatekeleza matakwa ya Sheria inayosimamia michezo hiyo katika uendeshaji wake na kuhakikisha Bahati Nasibu ya Taifa inakidhi matarajio ya kuanzishwa kwake kwa kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania.
“Bahati Nasibu ya Taifa ni zaidi ya mchezo wa kubahatisha, kwani ni fursa muhimu ya uwezeshaji wa kiuchumi na maendeleo ya jamii ikiwemo kukuza vipaji vya michezo na kama ilivyobainishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GBT, Mhe. Balozi Modest Mero, asilimia hamsini (50%) ya mapato yatakayokusanywa kupitia kodi za mchezo huu, yataelekezwa katika kukuza na kufadhili shughuli za maendeleo ya michezo nchini na Ushirikiano huu unashikilia maono ya pamoja yanayounganisha Serikali, waendeshaji, na washiriki katika kujenga mustakabali bora kwa wote” alisema Mhe Chande.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi ya GBT, Mhe. Balozi Modest Mero, alisema kuwa bodi ya wakurugenzi wa GBT, imeridhishwa na rekodi thabiti na uzoefu wa kampuni ya ITHUBA katika tasnia hiyo hasa katika uendeshaji wa Bahati Nasibu za Taifa katika nchi mbalimbali barana Afrika na wanaimani ni mshirika bora katika kuendesha Bahati Nasibu hapa Nchini.
“Kampuni hii imeonyesha uwezo na utayari wa kuleta Bahati Nasibu ya Taifa ambayo tulikuwa tunaikusudia na kuisubiria na hivyo sisi kama bodi tunashukuru sana ushirikiano na uungawaji mkono wa Serikali katika mradi huu kupitia Wizara ya Fedha” alisema Mhe. Balozi Mero.