Serikali kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imepanga kutoa jumla ya mitungi 100,000 bure ifikapo July,2023 katika maeneo ya Vijijini Nchi nzima ikiwa ni hatua ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Mpango huo umekuja mara baada ya Serikali kutenga Tsh. Bilioni 3.2 kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwaajili ya usambazaji wa gesi safi ya kupikia.
Akiongea Dar es salaam Mkurugenzi wa Uenezaji Masoko na Teknolojia Kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Advera Mwijage alipokutana na Wadau wa gesi nchini, amesema wameshaanza kuweka fomu ya maoni tangu Aprili 19 na kukamilishwa May 10,2023 ili kupata Watu watakaonufaika na gesi hizo.
Amesema nishati safi ni ile ambayo haichafui mazingira, inalinda afya ya Mwananchi lakini pia inatoa fursa kuwa kazi ya kupika ni starehe na isiwe shida hadi kufikia Mtu anapika huku anatoa machozi.
Mwaijage amesema Serikali ina mipango mingi kuhakikisha Wananchi wote wanafikiwa na nishati hiyo na licha ya kufikiwa wakiihitaji wapate kwa wakati.