Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameeleza Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa majengo yaliyo katika hali mbaya zaidi ndani ya Mji Mkongwe ambayo wananchi hawamudu gharama za kukarabati.
Rais Dk. Mwinyi amesema hayo leo tarehe 2 Disemba 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Mji Mkongwe wa Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Forodhani, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Dk. Mwinyi ametumia maadhimisho hayo kuishukuru Serikali ya Oman kwa kuungamkono kwa hali na mali juhudi za Zanzibar za kuuhifadhi Mji Mkongwe na maeneo mengine ya kihistoria yaliopo Zanzibar kwani msaada huo umechangia kuyaweka maeneo hayo kuwa endelevu wakati wote.
Aidha, Dk. Mwinyi amezipongeza Kampuni za Infinity, Maxbit na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mamlaka ya Mji Mkongwe.
Rais Dk. Mwinyi amesifu hatua ya Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa kuanzisha Mfumo wa kiditali aliouzindua katika kilele cha siku hiyo kwa uendeshaji wa mamlaka hiyo na usimamizi wa uingiaji wa watalii hatua itakayochangia kuongoza mapato ya Serikali na utoaji wa taarifa sahihi za Mji Mkongwe.
Waziri wa Utalii na mambo ya Kale Zanzibar Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga amesema mabadiliko chanya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane yameleta mabadiliko makubwa kwa Mji Mkongwe na kuuongezea umaarufu zaidi kimataifa.
Naye, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mji Mkongwe, Mhandisi Ali Said Bakari, ameishukuru Serikali ya Oman kwa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 25 kwa ukarabati wa jengo la Beit el Ajaab ambalo lina umuhimu kwa historia na Utalii wa Zanzibar.