Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali inaendelea kutoa kipaumbele kwa wanaosoma masomo ya Sayansi ikiwemo kutoa ufadhili wa masomo ili kuongeza hamasa kwa Vijana wa kitanzania wakiwemo wasichana kupenda kusoma masomo hayo.
Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo Februari 11, 2024 mkoani Arusha katika Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, ambapo amesisitiza kuwa serikali pia itaendelea kuwekeza katika mazingira mazuri kwa ajili ya Vijana kupata fursa mbalimbali katika nyanja za Sayansi za masomo na kuendeleza ubunifu ili kuendana na kasi ya teknolojia duniani na hata soko la ajira ndani na nje ya nchi.
“Taifa lina upungufu wa Wanasayansi na hasa Wanawake na Wasichana, kwa sababu ni wachache wanaosoma ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu (STEM) hivyo tutaendelea kuhamasisha wasichana kupenda na kujiunga na masomo hayo”. Alisema Mkenda.
Ameongeza kuwa ili Taifa liendelee linahitaji Wanasayasi hivyo Wizara na Wadau mbalimbali wataendelea kufungua fursa na kuweka mazingira sahihi ya ujifunzaji katika Sayansi.