Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi itaanza Mpango wa Utoaji wa Chanjo na utambuzi wa Mifugo Kitaifa kuanzia Mwezi Januari 2025 ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mpango huo unaolenga kudhibiti na kutokomeza magonjwa ya mifugo nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa Kampeni ya Chanjo za Mifugo Kitaifa uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete leo Desemba 18, 2024 jijini Dodoma, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) amesema mpango huo utakaotekelezwa kwa miaka mitano kutoka 2024-2029 na kugharimu Shilingi Bilioni 216 zitakazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Shilingi Bilioni 28.1 zitatumika awamu ya kwanza ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kuanzia Mwezi Januari 2025.
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeridhia kugharamia mpango wa chanjo wa miaka mitano kuanzia mwaka 2024 hadi 2029 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 216 kwa ajili ya uchanjaji na utambuzi wa mifugo kote nchini na mpango huu tutaanza Januari 2025 ambapo katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 28.1 kuchanja mifugo dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ng’ombe, Ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Ugonjwa wa Mdondo wa Kuku ili kuwasaidia wafugaji wetu kote Nchini” alisema Dkt. Kijaji.
Dkt. Kijaji amesema awamu ya kwanza ya mpango huo wa chanjo Serikali kupitia wataalamu wa Sekta ya Mifugo na Mamlaka za Serikali za Mitaa itachanja ng’ombe 19,097,223 dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Mapafu ya ngo’mbe (CBPP), Mbuzi na Kondoo 20,900,000 dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (PPR) na Kuku wa asili 40,000,000 dhidi ya Ugonjwa wa mdondo wa kuku (ND) ambapo lengo la serikali ni kutoa chanjo kwa mifugo angalau asilimia 70 ya idadi ya mifugo husika kwa miaka mitano mfululizo.
“Lengo la serikali ni kuchanja mifugo kufikia angalau asilimia 70 ya mifugo husika ambapo kwa sasa hali ya uchanjaji kwa ng’ombe, Mbuzi na Kondoo ni asilimia 21, Kuku wa Kienyeji asilimia 40 na kuku wa kisasa ni asilimia 100, hivyo kampeni hii itasaidia kutokomeza magonjwa ya mifugo, kutoa ajira za muda mfupi kwa vijana na wanawake 3540 na kuongeza usafirishaji wa nyama nje ya nchi Kutoka asilimia 14 ya sasa na kufikia asilimia 30 ifikapo mwaka 2029” alisema Dkt.Kijaji.
Dkt. Kijaji amesema katika kufanikisha zoezi la chanjo ya mifugo serikali itachangia nusu bei ya gharama za chanjo ili kuwarahisishia wafugaji kuchanja mifugo yao.
“Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuwa Serikali itachangia nusu ya bei kwa ajili ya chanjo kwa mifugo ambapo kwa upande wa Ng’ombe itachangia Shilingi 500, kwa upande wa mbuzi na kondoo itachangia Shilingi 300 na upande wa kuku itakchangia Shilingi 100 itakuwa sawa na bure” aliongeza Dkt. Kijaji.
Amehitimisha hotuba yake kwa kuwataka viongozi wa mamlaka ya serikali za mitaa, manispaa na majiji kutoa ushirikiano kwenye kampeni hiyo ya chanjo na kisha kueleza umuhimu wa chanjo za mifugo kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema Zoezi hilo la chanjo litahusisha wataalam na wafugaji katika kufanikisha hilo hivyo amewaomba wataalam na wafugaji kutoa ushirikiano wa zoezi hilo .
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Taifa CCWT Ndg. Mrida Mshota amesema zoezi la chanjo linalokuja kwa awamu hii litawasaidia mafugaji hasa kukabiliana na ugonjwa yaifugo na kuiomba Wizara kuupa kipaumbele pia ugongwa wa Miguu na midomo (FMD) na kisha kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania kuipa uzito na kipaumbele Sekta ya Mifugo.