Serikali kupitia Wizara ya Fedha inatarajia kukusanya sh bilioni 100 kila mwaka kutokana na uwekezaji wa dola 20 milioni uliofanywa na kampuni ya ITHUBA Tanzania, iliyopata leseni ya miaka nane kuendesha Bahati Nasibu ya Taifa.
Akizungumza Dar es Salaam leo Jumanne Januari 21, 2025 katika hafla ya kutambulisha uwekezaji huo, Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Hassan Chande, amesema serikali itachukua asilimia 18 ya fedha za washindi, pamoja na mapato mengine yatokanayo na mkataba huo.
“Uwekezaji huu utaimarisha sekta ya bahati nasibu nchini na kuchangia mapato ya taifa, huku ukiwa na manufaa kwa jamii,” amesema Chande.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe, amesema mradi huo utaongeza ajira zaidi ya 1,000 na kuboresha sekta ya michezo kupitia programu za kurudisha kwa jamii.
Naye Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania, Kelvin Koka, amesema kampuni yao inalenga kuboresha ukusanyaji wa mapato na maisha ya washiriki wa bahati nasibu kwa kuweka uwazi na mazingira shirikishi.