SERIKALI imesema itatumia mfumo wa ushirikiano na sekta binafsi (PPP) katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (BRT) na mwezi ujao watoa huduma watatu wataleta mabasi yao ili kuondoa tatizo la usafiri lililopo hivi sasa.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema Dar es Salaam ina tatizo la mabasi ya mwendokasi na serikali imeshafanya uamuzi — inatumia sekta binafsi kuongeza mabasi katika mradi huo.
“Tunatarajia mwezi wa tatu (Machi) watoa huduma wataanza kuleta hayo mabasi, tumepata watoa huduma watatu kwenye ile barabara mpya ya kwenda Mbagala, huko kuna maswali mengi sana. Watoa huduma wataleta mabasi mengi na ya kutosha lakini pia UDART (Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka) nao wanaongeza mabasi 150.
“Tunaamini haya yote yakiingia huko na wakati serikali inaendelea kufanya kazi na sekta binafsi, tunaamini msongamano kwa Jiji la Dar es Salaam utapungua kwa kiasi kikubwa na uwekezaji mkubwa unaoendelea Dar es Salaam wa barabara zile na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka yanafungua maeneo mengi,” alisema.
Kuhusu mvutano wa mabasi kutofika Kibaha, Msigwa alisema serikali inalifahamu na inalifanyia kazi. Muda si mrefu yataendelea kutoa huduma.