Serikali ya Korea Kaskazini imedai kuwa takribani Raia 800,000 wamejitolea kujiunga au kujiandikisha katika Jeshi la Taifa hilo kwa dhamira ya kupambana na Jeshi la Marekani kwa kile wanachodai kuchoshwa na uchokozi wa Marekani usioisha.
Takriban Wanafunzi na Wafanyakazi 800,000 kwa siku ya Ijumaa pekee walifunguka na kusema walitaka kujiandikisha na kulitumikia Jeshi la Taifa ili kukabiliana na Marekani, Gazeti la Serikali la Korea Kaskazini Rodong Sinmun limeripoti Wikiendi hii.
Madai hayo yamekuja baada ya Korea Kaskazini kurusha kombora la Hwasong-17 (ICBM) kujibu mazoezi ya kijeshi ya Marekani na Korea Kusini yanayoendelea, Makombora ya aina ya ICBM ya Korea Kaskazini yamepigwa marufuku chini ya maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na zoezi hilo lililaaniwa na Serikali za Korea Kusini, Marekani na Japan.
Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un anaishutumu Marekani na Korea Kusini kwa kuongeza mvutano baina yao kwa kitendo cha wao kufanya mazoezi ya kijeshi pamoja.