Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Habari vya Kielektroniki vya Pakistan (PEMRA) imezipiga marufuku chaneli za televisheni kurusha hewani hotuba za aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Imran Khan.
Hii ni baada ya kumtuhumu waziri mkuu huyo wa zamani kwamba anazishambulia taasisi za serikali na kuchochea chuki ndani ya nchi.
PEMRA imetangaza marufuku hiyo baada ya Khan kutoa hotuba katika mji wa mashariki wa Lahore, ambapo alidai kuwa mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Qamar Javed Bajwa ndiye aliyesababisha yeye kuondolewa madarakani Aprili mwaka jana.
Mwanasiasa huyo alitoa hotuba hiyo baada ya polisi kutoka mji mkuu Islamabad kujaribu kumkamata katika kesi ya rushwa.
Katika taarifa yake, Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Habari vya Kielektroniki vya Pakistan imesema, Khan anatoa madai yasiyo na msingi na kueneza matamshi ya chuki kupitia kauli zake za uchochezi dhidi ya taasisi na maafisa wa serikali jambo ambalo linaathiri udumishaji wa sheria na utulivu na kuna uwezekano wa kuvuruga amani na utulivu wa umma.
Hii ni mara ya tatu kwa PEMRA kupiga marufuku vituo vya televisheni kutangaza hotuba na taarifa za Imran Khan tangu alipopoteza uwaziri mkuu na kuanza kufanya mikutano ya hadhara kudai uchaguzi mkuu wa mapema.