Serikali ya Taliban imetangaza rasmi kuwa, kwa mujibu wa hukumu ya kiongozi wake Mullah Hebatullah Akhundzadeh, kuanzia sasa kilimo cha mmea wa bangi ni marufuku nchini humo, na kwamba ikiwa itashuhudiwa kilimo cha mmea huo kinafanyika mahali popote pale ndani ya Afghanistan wahalifu watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Tangu asili na jadi bangi inazalishwa kwa sura ya madawa ya kulevya nchini Afghanistan, lakini katika baadhi ya nchi duniani mmea huo hivi sasa unatumiwa kama dawa na kwa shughuli za viwandani.
Mwaka uliopita wa 2022, kiongozi wa Taliban Mullah Hebatullah Akhundzadeh alipiga marufuku kilimo cha mipopi pamoja na uzalishaji, ununuzi na uuzaji wa mihadarati ya kasumba inayotokana na mimea hiyo.
Afghanistan ni moja ya wazalishaji wakubwa na wakuu wa mihadarati duniani na huku zaidi ya watu milioni nne wakiwa ni waraibu wa madawa ya kulevya na zaidi ya wengine laki tano wanajishughulisha na upandaji, biashara na usafirishaji kimagendo wa mihadarati nchini Afghanistan.
Raia wa Afghanistan wanaamini kuwa, uzururaji wa waraibu wa madawa ya kulevya kwenye maeneo ya umma unasababisha adha kubwa na usumbufu kwa watoto na wanawake, wizi wa mali za watu na kuenea magonjwa mbalimbali, na wanataka serikali ichukue hatua kali zaidi za kupambana na janga hilo.