Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kuokoa zaidi ya TSH. trilioni 3.4 baada ya kufanikiwa kushinda mashauri mbalimbali yaliyofunguliwa na Watu binafsi,mashirika na taasisi dhidi ya Serikali .
Akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa Baraza la wafanyakazi mwaka wa fedha 2023/2024 Mkoani Morogoro Wakili mkuu wa Serikali Dokta Boniphace Luhende amesema ofisi hiyo imepata mafanikio makubwa katika utendaji Kazi wake ikiwemo kuokoa Kiasi hicho cha fedha Cha TSH. trilioni 3.4.
Dokta Luhende anasema endapo ofisi ya Wakili mkuu wa Serikali ingeshindwa katika mashauri hayo Serikali ingepata hasara Kubwa ambapo amebainisha mafanikio hayo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya menejimenti na wafanyakazi wa ofisi hiyo.
Anasema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wanakadiria kutumia bajeti ya Bil.20.7 tofauti na mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo walikua na makadirio ya bajeti Bil.17 hii ni kutokana na kuongeza wafanyakazi pamoja majukumu ya ofisi.
Anasema wafanyakazi wataendelea kufanya Kazi Kwa uadilifu na uaminifu ili kusaidia Serikali katika masuala ya kisheria .
Aidha ameshauri Serikali kuacha kuvunja mikataba ya wawekezaji na wakandarasi bila kushirikisha ofisi hiyo na ile ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwani inaleta changamoto katika ya masuala ya kisheria .
Kwa upande wake naibu waziri katiba na sheria Mhe. Jumanne Sagini amesema mikutano ya baraza la wafanyakazi lina umuhimu kwani linasaidia kutatua changamoto ya wafanyakazi Kwa kupatiwa ufumbuzi.
Mhe. Sagini amesema serikali imedhamiria kuondoa vitendo vya rushwa kazini hivyo kila mfanyakazi atimize wajibu wake kwa kufanya Kwa haki na weredi ambao unasaidia gurudumu la maendeleo.
Anasema wafanyakazi wa Ofisi ya Wakili mkuu wanatakiwa wajengewe uwezo mara kwa mara ili kuongeza ufanisi katika Utendaji Kazi hususani kipindi hiki ambacho nchi inatarajia kuingia katika zoezi la uchaguzi kwa mwaka 2024 na mwaka 2025.
Aidha ameipongeza ofsini hiyo kuweza kuokoa kiasi Cha fedha Cha zaidi ya trilioni 3.4 baada ya kushinda mashauri mbalimbali yaliyofunguli dhidi ya serikali ambapo amesema ushindi huu ni ishara wizara ya katiba na sheria inafanya vizuri.