Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), imepanga kupanua Barabara za kuingia na kutoka katikati ya jiji la Dodoma zenye jumla ya urefu wa kilometa 220 kwa kuzijenga kwa njia nne na sita kwa lengo la kuhakikisha jiji la Dodoma linaondokana na msongamano wa magari na kusaidia kuboresha huduma za usafiri na uchukuzi.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango na Miundombinu wa TANROADS, Mhandisi Ephatar Mlavi wakati akizungumza na waandishi wa habari wakati akielezea Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha Miaka minne inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Februari 17, 2025 katika Ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO.
Mhandisi Mlavi amezitaja barabara hizo kuwa ni Barabara ya Dodoma – Morogoro ambayo itajengwa (km 70), Dodoma – Arusha (km 50), Dodoma – Singida (km 50) na Dodoma – Iringa (km 50).
“Nia ni kuhakikisha barabara hizi zinaungana kwa urahisi na barabara ya mzunguko wa nje ya Dodoma ‘Dodoma Outer ring Roads’ na hivyo kulifanya jiji la Dodoma kuwa la mfano lisilo na msongamano wa magari na hivyo kuvutia shughuli za ukuaji wa uchumi”, amesema Mhandisi Mlavi.